Siku ya Tisa

*Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.*

Ninakuja mbele yako, Ee Mtakatifu Rita, siku hii ya mwisho ya Novena hii takatifu. Ninayasikia mapigo ya moyo katika kipindi hiki kigumu cha maisha yangu yaliyogawanyika. Ninaamini kwamba ombi langu litatimizwa na Bwana kupitia maombezi yako matakatifu. Lakini ikiwa haiwezekani, ninapaza sauti nikiomba kwa nguvu huruma na faraja yako. Usiniache niondoke bila kupata faraja yako.
Ee Mtakatifu Rita, ninaomba unifariji kwa mastahili ya mateso uliyoyapata hapa duniani na katika upweke wako wa sala. Unifariji kwa mastahili ya ukarimu uliokuwa nao kwa wenye shida. Unisikilize kwa mastahili ya upendo wako mkuu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa mama yake Bikira Maria Mtakatifu asiye na doa. Kwa mastahili ya ule mwiba Mtakatifu aliokujalia Bwana wetu Yesu Kristo, unisaidie na unifadhili mimi. Hiki ndicho kilio changu cha mwisho kwako wewe mama uliye Mtakatifu wa mambo yaliyoshindikana na mwombezi wa waliokata tamaa. Ninakuomba ujidhihirishe katika mwanga wako halisi, ili Mungu anijalie haya ninayoyaomba. Kwa msaada wako ninadhamiria kuachana na mwenendo wangu potofu, ili niwe mwenzaaji wa Nguvu za Mungu na uzuri wa mambo ya Mbinguni. Ninaahidi pia kuhiji mahali pako pa upweke, Ee Mtakatifu wa sala, huko Kashia, na au kwenye sanamu yako; ili niweze kuungana nawe katika kuabudu na kushukuru kwa fadhila za mbinguni nilizozipata kwa maombezi yako kutoka kwa Mwokozi wetu Azizi Yesu Kristo.

*Baba Yetu (3), Salamu Maria (3), Atukuzwe Baba (3)*

Kwa njia ya Mtakatifu Rita:- homa, madonda na tauni, viini vya maradhi mbalimbali, mapepo na ghadhabu vitoweke. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

Kwa maombezi yako:- radi, tetemeko la ardhi na moto havina nguvu. Kwa utakatifu wako mitego yote, hatari kubwa na vitisho vyote hutoweka. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

Hispania wanakutangaza kuwa Mtakatifu wa mambo yaliyoshindikana. Watu wengi wanaimba sifa zako. Kashia hutukuza jina lako. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

Kwa Mungu Mtakatifu, na kwa Mwanae ziwe sifa, utukufu na heshima, sifa kwa karne zote za pendo la milele. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

*K: Umemtia alama, Ee Bwana, mtumishi wako Rita.*
*W: Kwa mhuri wa upendo na mateso.*

*TUOMBE:* Ee Mungu, uliyekubali kumtawadha Mtakatifu Rita kwa neema, hata akakubali kuwapenda adui zake hadi akapata rohoni mwake na katika paji la uso alama za upendo na mateso. Tunakuomba kupitia maombezi yake, neema za kusamehe adui zetu na kutafakari maumivu ya mateso yako, ili tupate tuzo ulilotuahidia kwa wapole na wanaoteseka. Unayeishi na kutawala, daima na milele. Amina.

Baada ya kumaliza sehemu hii, sali Litania ya Mt. Rita, Litania ya Mwiba wa Mt. Rita, Zaburi ya 51 au Zaburi 130