Siku ya Tano

*Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.*

Ewe mchumba mpendwa wa Yesu, Mtakatifu Rita wa Kashia. Nakuja kwako tena. Nipo miguuni pako. Navutwa na wema wako kwa roho zenye kutaabika na kusumbuka. Unauona moyo wangu ulivyopondwapondwa kwa magumu ya dunia hii. Sipati tena tabasamu la thamani, roho yangu imevamiwa na mashaka mabaya, imani imetetereka na mshituko wa kukata tamaa kama msituko wa kifo unapiga miayo miguuni pangu. Nielekeze, Ee Mtakatifu mpendwa, nifanye nini katika mazingira haya ya kutisha? Nishauri nimwendee nani katika hali hii ya hatari katika maisha yangu? Kama kweli wewe ni Mtakatifu wa hali zote za kukatisha tamaa, njoo unisaidie kwani najisikia nimepotea. Nakuja kwako wewe ambaye kila mara wawahurumia wanaoteseka. Nakuja kwako unisaidie. Je, hutanionea huruma kutokana na hali yangu? Mtakatifu Rita najua u mwema sana. Najua hivyo, ndiyo maana najiweka mikononi mwako kwa moyo wangu wote ili unijibu kwa njia ya Yesu, lile ombi langu ambalo kwa imani kubwa naliomba **(hapa omba hitaji lako unalotaka kumwomba Mungu kupitia Mtakatifu Rita).**

*Baba Yetu (3), Salamu Maria (3), Atukuzwe Baba (3)*

Kwa njia ya Mtakatifu Rita:- homa, madonda na tauni, viini vya maradhi mbalimbali, mapepo na ghadhabu vitoweke. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

Kwa maombezi yako:- radi, tetemeko la ardhi na moto havina nguvu. Kwa utakatifu wako mitego yote, hatari kubwa na vitisho vyote hutoweka. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

Hispania wanakutangaza kuwa Mtakatifu wa mambo yaliyoshindikana. Watu wengi wanaimba sifa zako. Kashia hutukuza jina lako. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

Kwa Mungu Mtakatifu, na kwa Mwanae ziwe sifa, utukufu na heshima, sifa kwa karne zote za pendo la milele. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

*K: Umemtia alama, Ee Bwana, mtumishi wako Rita.*
*W: Kwa mhuri wa upendo na mateso.*

*TUOMBE:* Ee Mungu, uliyekubali kumtawadha Mtakatifu Rita kwa neema, hata akakubali kuwapenda adui zake hadi akapata rohoni mwake na katika paji la uso alama za upendo na mateso. Tunakuomba kupitia maombezi yake, neema za kusamehe adui zetu na kutafakari maumivu ya mateso yako, ili tupate tuzo ulilotuahidia kwa wapole na wanaoteseka. Unayeishi na kutawala, daima na milele. Amina.

Baada ya kumaliza sehemu hii, sali Litania ya Mt. Rita, Litania ya Mwiba wa Mt. Rita, Zaburi ya 51 au Zaburi 130