Siku ya Kumi na Mbili

*Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.*

Ee Mungu wangu mpendwa, ambaye huwaachi wenye kukutumaini na wenye kukuamini wapate mateso. Bali kwa upendo wasikiliza sala zao. Toka kilindini mwa moyo wangu nakutolea shukrani zangu za daima kwa fadhila ulizonijalia kwa maombezi ya mtumishi wako uliyemchagua, Mtakatifu Rita. Pokea, Ee Bwana Yesu shukrani zangu za dhati, zitokazo kama harufu nzuri ya sadaka. Pokea kupitia mikono ya Mtakatifu Rita. Ee Yesu mpenzi, nisaidie ili daima niwe macho kupokea ukarimu wako, wema wako na huruma yako.

Pamoja nawe, Ee Mtakatifu matenda miujiza, ambaye jina lako linatukuzwa kwa furaha kubwa duniani kote, na ambaye maombezi yako huleta miujiza; pokea shukrani zangu toka kilindini mwa moyo wangu. Ningetamani kila mtu akujue; watu wote wakupende. Kwani watu wote wangetambua nguvu zako za mbinguni. Ee nyota angavu ya Shirika la Mtakatifu Augustino; katika kutoa shukrani kwa mema niliyopata kwa fadhila nyingi, nitaeneza kwa watu wote ibada yako; nikiwaambia watu kuwa wewe kweli ni Mtakatifu wa mambo yaliyoshindikana, mwombezi wa waliokata tamaa, na mwombezi wa wote waliopoteza matumaini ya dunia hii.

*Baba Yetu (3), Salamu Maria (3), Atukuzwe Baba (3)*

Kwa njia ya Mtakatifu Rita:- homa, madonda na tauni, viini vya maradhi mbalimbali, mapepo na ghadhabu vitoweke. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

Kwa maombezi yako:- radi, tetemeko la ardhi na moto havina nguvu. Kwa utakatifu wako mitego yote, hatari kubwa na vitisho vyote hutoweka. Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.

Hispania wanakutangaza kuwa Mtakatifu wa mambo yaliyoshindikana. Watu wengi wanaimba sifa zako. Kashia hutukuza jina lako. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

Kwa Mungu Mtakatifu, na kwa Mwanae ziwe sifa, utukufu na heshima, sifa kwa karne zote za pendo la milele. *Unawasaidia vipofu, viziwi, bubu na viwete: watoto wanaomba sana na wafu wanarudishiwa uhai.*

*K: Umemtia alama, Ee Bwana, mtumishiwako Rita.*
*W: Kwa mhuri wa upendo na mateso.*

*TUOMBE:* Ee Mungu, uliyekubali kumtawadha Mtakatifu Rita kwa neema, hata akakubali kuwapenda adui zake hadi akapatarohoni mwake na katika paji la uso alama za upendo na mateso. Tunakuomba kupitia maombezi yake, neema za kusamehe adui zetu na kutafakari maumivu ya mateso yako, ili tupate tuzo ulilotuahidia kwa wapole na wanaoteseka. Unayeishi na kutawala, daima na milele. Amina.

Baada ya kumaliza sehemu hii, sali Litania ya Mt. Rita, Litania ya Mt. Rita